Mtazamo wa mahari na utamaduni

MAHARI ni moja ya mila na desturi au utamaduni uliotapakaa sehemu kubwa ya sayari hii ya dunia kwa miaka mingi ambapo watu wengine wa kileo wanakubaliana nawo na wengine wakiuponda.

Na kila jamii ina utaratibu wake wa kutoza mahari, ima iwe kwa taratibu za kidini kikabila au vinginevyo, ilimradi lile lengo la kutoa mahari hiyo inakuwa imefikiwa na muhusika baada ya kukubaliana na taratibu husika

Pengine ni vema tujiulize mahari ni nini ? na jamii inalichukuliaje suala hili hasa katika taratibu za kimila kama inakidhi hali ya sasa

Kiujumla mahari ni aina ya  malipo anayolipwa binti au malipo yanayotolewa na upande wa mume anayetaka kuoa kwa wazazi wa binti au bi harusi mtarajiwa.

Kwa sehemu kubwa malipo haya hutofautiana kati ya kabila moja hadi jingine na kiasi au idadi hutegemea makubaliano baina ya pande mbili husika.

Kama ilivyo neno mahari kwa zamani ililenga neno mali kama vile mifugo ifugwayo katika jamii , kuku,mbuzi, ng’ombe, kondoo, punda, hata na bata, kabla ya mahari ya aina hiyo haijaathiriwa na utandawazi na kwa miaka ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na muingiliano wa makabila  hali iliyopelekea watu kulipana kwa njia ya fedha zinazothamanishwa na idadi ya mifugo.

Utafiti mbali mbali umebaini  kuwepo makundi ya watu wenye mitazamo tofauti kuhusu suala hili la mahari ambapo baadhi ya watu  wasioona umuhimu na faida ya utaratibu huu wanadai kuwa unawafanya vijana wengi washindwe kufikia lengo la kuoa kwa kuogopa gharama za kulipa mahari.

Wenye misimamo hii wanadai mahari yanawadhalilisha mabinti kwani wanakuwa kama wameuzwa kwa wanaume kitendo wanachokitafsiri kama kuuendeleza utumwa na biashara ya binadamu.

Mzee Hasan Bulegi mkazi wa Utete Mkoani  Pwani anasema suala la mahari hasa kwa mtu kutajiwa kiwango kikubwa na upande wa mwanamke ni sababu tosha ya kuwafanya vijana wengi waishi katika hali ya kutokuwa na ndoa

“Ndoa ni makubaliano baina ya watu wawili mwanamke na mwanaume na kisha ndiyo wanashirikisha familia za pande zote mbili, kwa ajili ya kutambuana sasa upande mmoja unapotaka kumfanya mwanae kama kitega uchumi ni hatari kwa maendeleo ya vijana wao wakishaingia katika ndoa”anasema mzee Bulegi

Mawazo yake yanaungwa mkono na Jafari Mhando Mkazi wa mlandizi anayesema suala la mahari kupangwa na ukoo ni tatizo na kikwazo kwa vijana wengi kuweza kutimiza malengo yao ya kuoa, kwa kuwa yanawanyima fursa ya kupanga maisha yao ya baadae kwa ajili ya kiasi kikubwa kilichotoka katika mahari.

“Mimi nimeachana na mpenzi wangu wa kwanza kwa sababu waliniambia mahari ni shilingi 350000/= hapo bado suala la sherehe baina yetu na jukumu lote hilo nilitakiwa kulibeba mimi, wakati awali tulikubaliana binti asomewe dua tu”anasema Mhando

Mitazamo ya bulegi na Mhando inazidi kufanana kwa kuwa wote wanaona sula hilo ni la kuwadhalilisha mabinti  kwani wavulana wanajisikia kama wamewanunua wake zao kwa gharama ya walizotajiwa

Wapo watuwanao tetea uwepo wa mahari wanasema kwamba utamaduni wa kulipana mahari ni wa siku nyingi na unapaswa kuendelea kuheshimiwa na watanzania ili kuhifadhi mila zetu.

Wanaendelea kusema kuwa mahari yanawafurahisha wazazi wengi kwa kuamini kuwa  angalau watakuwa wamepunguza gharama walizopata wakati wakimkuza binti yao tangu utotoni .

“Ni lazim tupange mahari kwa maana ndoa ya sasa ni sehemu ya maisha na ni kama kamari, kwa vilewengine tunakuwa tumewasomesha binti zetu kwa gharama kubwa na kumpatia mafanikio mbali mbali sasa anapoenda kwa mume anakuwa tayari amemrahisishia maisha” anasema adili kiwelu ambaye binti yake mmoja anasoma katika moja ya vyuo vikuu nje ya nchi.

Kwa upande mwengine mahari ni ishara nzuri kwa binti anayetaka kuolewa kuamini kuwa hakika mvulana wake  yuko makini katika kujenga ndoa yao na siyo mlaghai

Hata hivyo kundi lingine lisiloafiki kuendelea na utamaduni huu lina maoni hasi  na  kudai kuwa ni utaratibu uliopitwa na wakati na yafaa kwa watu wasiojua kuzisoma nyakati.

Wanadai kuwa  mahari  hufanya ndoa ya kiuchumi zaidi kuliko hali ya msukumo wa upendo ambao ndio chimbuko la wawili  kutamani kuishi pamoja katika maisha kama mume na mke.

Katika hali hii mahari yanakuwa  ishara kwamba wenye uwezo wa kifedha au mali nyinginezo ndiyo  wawezao kuoa.

Kundi hili pia linapigilia msumari kama wana harakati wa kutetea haki za wanawake wakidai kwamba biashara ya kubadilishana pesa au ng’ombe kwa binti ni udhalilishaji mkubwa wa jinsia hii ya kina mama kwa kuwafanya kama bidhaa sokoni. Aghalabu kupitia utamaduni huu wa kulipana mahari  wazazi wamekuwa wakihesabu kuwa kuzaa watoto wa kike ni ishara chanya kuwa utajiri umeingia nyumbani.

Hata kama mwanamke atashindwa kuvumilia maisha ya ndoa na mumewe kamba ya mahari kwenye ndoa yao humfanya ashindwe kuvunja ndoa hiyo na hivyo kuishi chini ya shinikizo la mahari.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: